Abstract:
IKISIRI
Ken Walibora amewaumba wahusika wa kiutopia katika riwaya zake. Utafiti huu ulikusudia kubainisha ikiwa wahusika katika riwaya za Walibora wanawakilisha uhalisia wa jamii. Lengo kuu katika utafiti lilikuwa kubainisha upekee wa baadhi ya wahusika katika riwaya teule za Ken Walibora. Utafiti uliongozwa na madhumuni matatu. Kwanza utafiti ulidhamiria kudadavua uhalisia wa baadhi ya wahusika katika riwaya teule za Ken Walibora. Maudhui ya pili yalikuwa kupambanua mbinu za utunzi zilizohusika katika kuwajenga wahusika wa kipekee, na ya mwisho kufafanua jinsi maudhui anuwai yalivyojenga sifa tabia za wahusika. Sababu kuu ya kuchagua mada hii ni kuwa, baadhi ya watunzi wa riwaya za Kiswahili huumba wahusika kwa njia ya kipekee na kuwafanya waonekane viumbe wasio wa kawaida. Utafiti huu ulitathmini ikiwa wahusika hao huakisi hali halisi katika jamii. Utafiti huu ulikuwa wa maktabani. Nilifanya uteuzi wa sampuli kimaksudi na kusoma riwaya teule za Walibora kwa upekuzi na kunakili data iliyokusudiwa. Data iliyohusiana na utafiti huu kutoka makala mbalimbali ilikusanywa kutoka maktaba ya vyuo na intaneti na kutumika katika uchanganuzi wa data kwa mbinu ya kimaelezo. Utafiti huu uliongozwa na nadharia za mwitikio wa msomaji iliyoasisiwa na Stanley Fish, James Tompkins, Robert Jauss, Rosenblatt na Wolfgang. Matokeo ya utafiti huu yalibainisha kuwa Walibora amewasawiri wahusika wakiwa viumbe wasio wa kawaida na kwa njia ya kipekee kuakisi hali halisi ya jamii. Matokea ya utafiti huu yatakuwa ya muhimu katika kuwaelewesha wasomaji namna wahusika huumbwa na kutumiwa na waandishi kupitishia ujumbe, kwa njia ya kipekee. Matokea ya utafiti huu yatakuwa ya manufaa kwa wasomi wa fasihi ya Kiswahili hasa utanzu wa riwaya. Pia yatakuwa daraja kwa wale watakaofanya utafiti kama huu baadaye.